Elizabeti (au Elisabeti, kwa Kiebrania אֱלִישֶׁבַע / אֱלִישָׁבַע, Elišévaʿ; kwa Kigiriki Ἐλισάβετ, Elisabet; kwa Kiarabu أليصابات, Alyassabat; maana yake ni "Mungu ameapa") alikuwa mwanamke wa ukoo wa Haruni aliyeolewa na Zakaria, kuhani mwaminifu wa Israeli katika karne ya 1 KK.
Hawakupata mtoto hadi uzeeni kutokana na utasa wa Elizabeti, lakini hatimaye walijaliwa kumzaa Yohane Mbatizaji.
Wote wanaheshimiwa kama watakatifu. Sikukuu ya wazazi ni tarehe 5 au 23 Septemba[1], kadiri ya madhehebu. Pengine wanaheshimiwa pamoja na mtoto wao tarehe 24 Juni.
Habari hizo zinapatikana hasa katika Injili ya Luka, sura ya 1 na ya 2. Humo inaelezwa Zakaria alivyopashwa na malaika Gabrieli kwamba atapata mtoto wa kiume ambaye atakakuwa nabii mkuu na kumtangulia Bwana[2].
Ingawa Zakaria hakusadiki mara, na kwa sababu hiyo aliadhibiwa kwa kufanywa bubu na kiziwi hadi ahadi itimie, siku ya kumtahiri mtoto alifungua tena kinywa chake na kutoa unabii.
Katikati ya matukio hayo, Elizabeti alitembelewa na jamaa yake, Bikira Maria, akiwa pia mja mzito[3]. Kabla ya kuongea lolote, salamu ya Maria ilimfanya Yohane aruke kwa shangwe tumboni mwa mamaye, na kusababisha Elizabeti atambue hali ya Maria na kumtolea kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu maneno ya sifa kwa imani yake na ujauzito wake wa pekee.
Hata Kurani inamzungumzia bila kumtaja kwa jina, ikieleza Mungu alivyoponya utasa wake aweze kumzaa nabii Yahya, hasa katika sura ya 21.
![]() |
Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Elizabeti (Injili) kama habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |