Eneo la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere nchini Tanzania.

Hifadhi ya Taifa ya Nyerere (awali: Selous, matamshi: "saluu") ni hifadhi ya taifa kubwa kuliko yote nchini Tanzania, pia ni kati ya hifadhi ya wanyama kubwa kabisa duniani. Hifadhi imeanzishwa mwaka wa 2019; kabla ya kupandishwa hadhi na kuwa hifadhi, ilikuwa pori tengefu lililojulikana kwa jina la Selous.

Eneo lake ni la km² 54,600 katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Eneo hilo ni kubwa kushinda nchi 70 duniani ikikadiriwa kuwa na eneo sawa na nchi ya Kostarika (Amerika ya Kati) na takribani mara mbili kuliko nchi ya Ubelgiji (Ulaya).

Sehemu kubwa ya eneo iko katika hali ya asili bila kuvurugwa na shughuli za binadamu. Tangu mwaka 1982 imeingizwa katika orodha ya UNESCO ya Urithi wa Dunia. Tena mwezi Juni 2014 imeingizwa kwenye orodha ya UNESCO ya hifadhi zenye hatari ya kupotewa na uhai wake.

Jina

Jina la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere limechaguliwa kwa heshima ya mwanzilishi wa Taifa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Jina la awali lilitokana na Mwingereza Frederick Selous aliyekuwa mwindaji wakati wa kuanzishwa kwa ukoloni katika Afrika ya Kusini na Mashariki na ambaye aliuawa katika Tanzania ya leo akiwa mwanajeshi wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Wanyama na mimea

Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ina aina kadhaa za wanyamapori wanaopatikana ndani yake: kati yao ni: simba, nyumbu, twiga, pundamilia, kiboko, kifaru, swala, fisi, mbwa mwitu wa Afrika, na idadi kubwa ya mamba wanaopatikana katika mto Rufiji. Hao wote wanaweza kuonekana wakati wa kutembelea hifadhi hii. Hapo awali hifadhi ya Taifa ya Nyerere (Selous) ilikuwa nyumbani kwa tembo wengi sana lakini kwa sababu ya ujangili uliokithiri idadi imepungua sana.

Namna ya kufika

Picha

Tazama pia

Marejeo

  1. "Nyerere National park". Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2020-11-25. Iliwekwa mnamo 2020-11-22. 

Majarida ya hifadhi za Taifa Tanzania

Viungo vya nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Hifadhi ya Taifa ya Nyerere