Miujiza ya Yesu ni matendo yapitayo sheria za maumbile[1] yaliyofanywa na Yesu kadiri yanavyosema maandiko matakatifu ya Ukristo na Uislamu. Ilikuwa mingi sana; hata hivyo Injili ya Yohane (21:25) inashuhudia kwamba michache tu imeandikwa.[2][3][4]
Kati ya miujiza hiyo, kuna mazinguo ya kufukuza pepo wachafu, uponyaji wa maradhi mbalimbali (homa, ukoma, safura, kupooza mkono au mwili mzima, kupinda kwa mgongo, kutokwa damu mfululizo, upofu, uziwi, ububu na vilema vingine), ufufuo wa wafu, na ushindi juu ya uasilia (kama kugeuza maji kuwa divai, kutembea juu ya maji ya ziwa, kutuliza dhoruba na kuzidisha mkate na kitoweo cha samaki).[5][6]
Kwa Wakristo na Waislamu, miujiza kama hiyo ilitokea kweli.[7]
Baadhi ya wataalamu wanatoa hoja ili kuthibitisha hilo.[8][9]
Kama kawaida, watu wengine wanakanusha dai hilo au wanasema miujiza ni mifano ya mambo ya kiroho tu.[10]
Miujiza ilikuwa na umuhimu wake katika utume wa Yesu, ikishuhudia mamlaka yake ya Kimungu[3], kama vile njaa, kiu, uchovu na mateso vinavyoshuhudia ubinadamu wake.[11][12][13]
Pamoja na hayo, miujiza ilitokana pia na upendo na huruma yake kwa binadamu mwenye shida.[3][14]
Miujiza ililenga pia kutoa ujumbe kwa matendo ili kufafanua na kuthibitisha maneno kama vile haja ya kuwa na imani.[15][16] Kila muujiza ulikuwa na fundisho maalumu.
Vitabu vya kale (kuanzia karne ya 2) ambavyo havikukubalika katika Agano Jipya la Biblia ya Kikristo vinasimulia miujiza mingine ambayo Yesu aliweza kufanya tangu utotoni. Vitabu hivyo ni kama Injili ya Siri ya Marko 1, Injili ya Utoto ya Thoma 2.2, 2.3, 9-18, Injili ya Yakobo 19-20.
Sanaa ya Kikristo imechochewa na miujiza hiyo, kwa mfano katika michoro ifuatavyo.
![]() |
Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Miujiza ya Yesu kama historia yake au athari wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |