Kwa sarafu ya Uingereza, angalia makala ya Pauni (sarafu)
Ratili (kutoka Kiarabu رطل ratl; pia: pauni kutoka Kiingereza pound) ni jina la kizio cha uzito wa takriban nusu kilogramu.[1] Wakati wa ukoloni chini ya mfumo wa vipimo rasmi vya Uingereza wakati ule pound ilikuwa kipimo rasmi kilicholingana na gramu 454. Kifupi chake kilikuwa £ au lb kutoka Kilatini libra.
Tangu kuenea kwa vipimo vya SI ratili imetazamiwa kama jina la takriban gramu 454.
Ratili pia ni kati ya vipimo asilia vya Kiswahili. Kihistoria, ilikuwa kipimo cha uzito cha takriban nusu kilogramu au gramu 400-500.
Ratili ilipokewa kutoka vipimo vya Kiarabu رطل ratl, iliyotumiwa kwa jina hili katika sehemu nyingi za nchi za Kiislamu. Lakini uzito wa ratl ulikuwa tofauti kati ya nchi, majimbo na miji, kuanzia gramu 340 hadi zaidi ya kilogramu 2. Ratili ya Uswahilini ililingana zaidi na ratl jinsi ilivyotumiwa Uarabuni katika eneo la Makka iliyokuwa kidogo juu ya gramu 400.[2]
Hadi leo "ratili" inatumiwa pale ambako matini za kiingereza zinatafsiriwa zinazotumia pound.