| |||
Lugha rasmi | Kiitalia; kijimbo pia Kijerumani, Kifaransa, Kiladino, Kislovenia, Kisardinia | ||
Mji Mkuu | Roma | ||
Rais | Sergio Mattarella | ||
Waziri Mkuu | Mario Draghi | ||
Eneo | km² 302,072.84 | ||
Wakazi | 59,236,213 (31-12-2020) (23º duniani) | ||
Wakazi kwa km² | 201.7 | ||
JPT | 31,022 US-$ (2008) | ||
Pesa | Euro | ||
Wakati | UTC+1 | ||
Wimbo wa Taifa | Fratelli d'Italia (Ndugu wa Italia) | ||
Sikukuu ya Jamhuri | 2 Juni | ||
Sikukuu ya Ukombozi | 25 Aprili | ||
Simu ya kimataifa | +39 | ||
Jamhuri ya Italia (kwa Kiitalia: Repubblica Italiana) ni nchi ya Ulaya Kusini inayoenea katika sehemu kubwa ya Rasi ya Italia na baadhi ya visiwa vya jirani kwenye Bahari ya Kati.
Eneo lake ni km² 302,072.84 ambalo lina wakazi 59,236,213 (31-12-2020): ni nchi ya 23 duniani kwa wingi wa watu, lakini ya 8 au 9 kwa uchumi. Mtu anayetokea katika nchi hii ya Italia kwa Kiswahili huitwa Mwitalia.
Imepakana na Ufaransa, Uswisi, Austria na Slovenia. Nchi huru mbili ndogo zinazozungukwa na eneo la Italia pande zote ni San Marino na Vatikano.
Makao makuu ni jiji la Roma, lenye umuhimu mkubwa katika historia ya dunia nzima.
Umbo la jamhuri, kama lile la rasi yake, linafanana na mguu linalozungukwa na maji ya Mediteraneo pande tatu.
Milima ya Appennini inaunda uti wa mgongo wake, wakati ile ya Alpi, ambayo ni mirefu zaidi, inaunda kwa kiasi kikubwa mpaka kati ya Italia na nchi nyingine za Ulaya.
Mlima mrefu zaidi, ukiwa na mita 4,810 juu ya usawa wa bahari, unaitwa Monte Bianco (Mlima Mweupe) na uko mpakani kwa Ufaransa.
Visiwa viwili vikubwa vya Sisilia na Sardinia ni sehemu za Italia pamoja na visiwa vingi vidogovidogo, vile vya Pelagie vikiwa upande wa Afrika.
Italia ina volkeno 14, ambazo 4 kati yake ziko hai: ile ndefu zaidi kuliko zote za Ulaya (mita 3,329) inaitwa Etna na iko mashariki mwa Sisilia. Italia inaongoza Ulaya kwa wingi wa matetemeko ya ardhi.
Mto mrefu zaidi unaitwa Po na una urefu wa kilomita 652. Mito mingine mirefu ni Adige, Tevere, Adda, Oglio, Tanaro, Ticino, Arno, Piave, Reno, Sarca-Mincio n.k.
Maziwa makubwa zaidi ni: Garda (km2 367.94), Ziwa Maggiore (212.51, likiingia Uswisi), Ziwa la Como (145.9), Trasimeno (124.29) na Ziwa la Bolsena (113.55).
Kutokana na urefu mkubwa wa Italia toka kaskazini hadi kusini, hali ya hewa ni tofauti sana, kuanzia baridi kali sana hadi joto kali sana.
Bendera | Jina | Makao makuu | Eneo (km2) | Wakazi | Msongamano wa watu/km² | Wilaya | Miji | Miji mikubwa | Hali ya utawala |
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
Abruzzo | L'Aquila | 10,763 | 1,307,919 | 122 | 4 | 305 | - | Kawaida | |
Bonde la Aosta | Aosta | 3,263 | 126,933 | 39 | 0 | 74 | - | Kujitawala | |
Puglia | Bari | 19,358 | 4,045,949 | 209 | 6 | 258 | Bari | Kawaida | |
Basilicata | Potenza | 9,995 | 575,902 | 58 | 2 | 131 | - | Kawaida | |
Calabria | Catanzaro | 15,081 | 1,954,403 | 130 | 5 | 409 | Reggio Calabria | Kawaida | |
Campania | Napoli | 13,590 | 5,761,155 | 424 | 5 | 551 | Napoli | Kawaida | |
Emilia-Romagna | Bologna | 22,446 | 4,354,450 | 194 | 9 | 348 | Bologna | Kawaida | |
Friuli-Venezia Giulia | Trieste | 7,858 | 1,219,356 | 155 | 4 | 218 | Trieste | Kujitawala | |
Lazio | Rome | 17,236 | 5,550,459 | 322 | 5 | 378 | Rome | Kawaida | |
Liguria | Genoa | 5,422 | 1,565,349 | 289 | 4 | 235 | Genoa | Kawaida | |
Lombardia | Milan | 23,861 | 9,749,593 | 409 | 12 | 1544 | Milan | Kawaida | |
Marche | Ancona | 9,366 | 1,541,692 | 165 | 5 | 239 | - | Kawaida | |
Molise | Campobasso | 4,438 | 312,394 | 70 | 2 | 136 | - | Kawaida | |
Piemonte | Turin | 25,402 | 4,366,251 | 172 | 8 | 1206 | Turin | Kawaida | |
Sardinia | Cagliari | 24,090 | 1,637,193 | 68 | 8 | 377 | Cagliari | Kujitawala | |
Sisilia | Palermo | 25,711 | 4,994,817 | 194 | 9 | 390 | Catania, Messina, Palermo | Kujitawala | |
Trentino-Alto Adige/Südtirol | Trento | 13,607 | 1,036,707 | 76 | 2 | 333 | - | Kujitawala | |
Toscana | Firenze | 22,994 | 3,679,027 | 160 | 10 | 287 | Firenze | Kawaida | |
Umbria | Perugia | 8,456 | 885,535 | 105 | 2 | 92 | - | Kawaida | |
Veneto | Venisi | 18,399 | 4,865,380 | 264 | 7 | 581 | Venisi | Kawaida |
Akiolojia imethibitisha uwepo wa Homo neanderthaliensis miaka 128,000-187,000 hivi iliyopita. Homo sapiens sapiens alifika miaka 40,000 hivi iliyopita.
Kufikia milenia ya 1 KK wakazi wengi walikuwa wa jamii ya Kizungu na kutumia lugha za Kihindi-Kiulaya.
Peninsula ya Italia iliunganishwa mara ya kwanza na Jamhuri ya Roma (509-27 KK), lakini hiyo ilipoenea Ulaya kusini na magharibi, Afrika ya Kaskazini na Asia ya Magharibi ikawa na sura ya kimataifa kama Dola la Roma.
Umoja ulipotea kuanzia uvamizi wa jiji la Roma uliofanywa na Wagermanik (476 BK) na hasa baada ya ufalme wa Karolo Mkuu aliyetawala sehemu ya kaskazini tu.
Juhudi za kuurudisha umoja zilifanywa hasa katika karne ya 19, ambapo Ufalme wa Sardinia uliteka sehemu kubwa ya Italia (hasa miaka 1860, 1866 na 1870) na kubadilika kuwa Ufalme wa Italia wenye makao makuu Roma.
Baada ya vita vikuu vya pili iligeuka Jamhuri yenye katiba inayotia mamlaka kuu mikononi mwa bunge.
Ni kati ya nchi sita zilizoanzisha Umoja wa Ulaya mwaka 1957 ikaendelea kuunga mkono ustawi wake hadi uanzishaji wa pesa ya pamoja (Euro).
Italia ni kati ya nchi zilizoendelea, ikiwa na nafasi ya nane kwa nguvu ya uchumi duniani, hivyo ni mwanachama wa G7, G8 na G20.
Italia ndiyo nchi inayongoza duniani kwa kuwa na mahali pengi (51) pa kimaumbile na pa kihistoria palipoingizwa katika orodha ya UNESCO ya "Urithi wa Dunia".
Kwa sababu hiyo pia inashika nafasi ya 5 kati ya nchi zote zilizo lengo la utalii.
Wananchi wana sifa za pekee kati ya Wazungu wote, hata upande wa DNA, kutokana na jiografia na historia ya rasi.
Ni kati ya nchi ambamo watu wanatarajiwa kuishi miaka mingi zaidi, lakini pia ni kati ya nchi ambapo uzazi ni mdogo zaidi: wanaokufa ni wengi kuliko wanaozaliwa.
Kutokana na umati wa Waitalia waliohama nchi hiyo karne za nyuma, sasa zaidi ya watu milioni 60 nje ya Italia wana asili ya nchi hiyo, mbali na raia zaidi ya milioni 4 wanaoishi nje.
Lugha rasmi ni Kiitalia, inayotegemea zaidi lahaja za Italia ya Kati, lakini siku hizi inatumiwa na wananchi walio wengi hata katika mikoa mingine, ambayo kwa jumla ni 20.
Upande wa dini, wengi wao (81.2%) ni Wakristo wa Kanisa Katoliki, wakifuatwa na Waorthodoksi (2.8%, wengi wao wakiwa wahamiaji, hasa kutoka Romania) na Waprotestanti (1.1%, wengi wao wakiwa Wapentekoste). Uhamiaji mwingi wa miaka ya mwisho wa karne ya 20 umeleta pia Uislamu (3.7%) na dini nyingine.
Dini zote zinaachiwa uhuru na, tofauti na nchi nyingi za Ulaya, waumini wake wanajitahidi kiasi kufuata ibada (29% kila wiki).
((cite web))
: CS1 maint: date auto-translated (link)
((cite web))
: CS1 maint: date auto-translated (link)
((cite web))
: More than one of |accessdate=
na |access-date=
specified (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
((cite web))
: CS1 maint: date auto-translated (link)((cite web))
: CS1 maint: date auto-translated (link)((cite web))
: CS1 maint: date auto-translated (link) CS1 maint: unrecognized language (link)
Nchi za Umoja wa Ulaya | |
---|---|
Austria | Bulgaria | Eire | Estonia | Hispania | Hungaria | Italia | Kroatia | Kupro | Latvia | Lituanya | Luxemburg | Malta | Polandi | Slovakia | Slovenia | Romania | Ubelgiji | Ucheki | Udeni | Ufaransa | Ufini | Ugiriki | Uholanzi | Ujerumani | Ureno | Uswidi |
Makala hii kuhusu maeneo ya Italia bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Italia kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |