Jan Knappert (14 Januari 1927 – 30 Mei 2005) alikuwa mwanaisimu kutoka nchi ya Uholanzi mwenye umaarufu wa kimataifa, alikuwa mtaalamu hasa wa lugha za Kiswahili na Kiesperanto.
Alifundisha kwenye vyuo vikuu mbalimbali pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Nairobi, School of Oriental and African Studies katika Chuo Kikuu cha London, hadi kurudi Ulaya bara alipofundisha miaka mingi kwenye Chuo Kikuu cha Leuven.
Alikuwa pia na shahada za uzamili katika Kisanskrit, lugha za Kisemiti (pamoja na Kiebrania, Kiarabu na Uislamu), na lugha za Austronesia (pamoja na Kimalay, Kitagalog, Kihawaii na Kimalagasy)[1]
Katika miaka alipokaa Afrika ya Mashariki alikusanya miswada mingi ya Kiswahili iliyoandikwa kwa herufi za Kiarabu[2] akatumikia pia kama Katibu wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki.[3].
Alikabidhi mkusanyo wa miswada ya Kiswahili kwa Chuo Kikuu cha London.[4] ambako sehemu imeshapatikana kwa umma kwa njia ya intaneti.
Aliandika mengi na vitabu vingi. Utafiti wake kuhusu Kiswahili ulikazia hasa utamaduni, ushairi na dini ya Waswahili.
Alikusanya orodha ya istilahi za Kiswahili za kutaja nyota, makundinyota na sayari na hivyo kuhifadhi elimu ya vizazi Waswahili waliokuwa mabaharia na kuvuka bahari katika jahazi zao, ambayo ni elimu inayopotea haraka kutokana na mabadiliko ya teknolojia na ubaharia.[5].
Akiunganisha elimu yake ya lugha mbalimbali alitunga Kamusi ya Esperanto-Kiswahili akatafsiri pia utenzi wa kitaifa ya Kifini (unaoitwa Kalevala) kwa Kiswahili.
Baadhi ya vitabu vyake